Nchini Kenya, maafisa wengi wa polisi ni wanaume. Lakini katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na uhamasishaji wa haki sawa kwa wanaume na wanawake katika sekta mbalimbali. Jambo hili limechangia kuongezeka kwa maafisa wa kike katika idara ya polisi. Hata hivyo, kumezuka maoni tatanishi hasa kuhusu miili ya maafisa wa kike. Kutokana na maoni hayo yanayopatikana haswa mitandaoni, ni dhahiri kwamba wananchi huwachukulia maafisa wa kike kwa mzaha sana. Mtazamo huu wa wananchi unatoa wazo kuwa wanawaona maafisa hawa kwa jinsi tofauti ikilinganishwa na wenzao wa kiume.

Mfano mzuri wa kuwatia maafisa wa kike katika mizani mbadala unadhihirika katika mijadala katika mitandao ya kijamii. Miaka michache iliyopita, afisa mmoja wa kike alipata umaarufu usiomidhilika. Umaarufu huu uliendeshwa na kulengeshwa, sio kwenye kazi na juhudi zake katika kuimarisha ulinzi, bali ni kupitia urembo wa sura na umbile lake. Mwili wa afisa huyu ulijadiliwa, ukasifiwa, na kumezewa mate hadharani kwa siku kadhaa. Vile vile picha yake ilikatakatwa na kuhaririwa kwa jinsi tofauti ili kutosheleza matwaka ya wananchi haswa, nafikiri, wanaume. Ilishangaza sana kuona baadhi ya wanaume wakitamani hadharani kukamatwa na afisa huyo. Wengi walirai, “Tafathali nikamate!”

Vyombo vya habari navyo havikuchelea kumsaka na kumhoji afisa huyo. Katika mahojiano, afisa huyo hakuonekana kuudhika wala kuhisi vibaya kuhusu mijadala iliyoenea na kutandawaa kuhusu mwili wake. Badala yake, alitabasamu na kucheka tu huku akisema kwamba naye pia amajionea mijadala kumhusu na kuuhusu mwiliwe kwenye mitandao ya kijamii. Katika ripoti zao, waandishi wa habari na watangazaji hawakuonyesha mshangao wala kuona mijadala hiyo kama kinyume na kawaida. Kwao, mijadala hii ilikuwa utani tu na mizaha isiyokuwa na ubaya wala madhara yoyote.
Ni jambo la kawaida na la kutarajiwa kabisa hadi sasa kwa maafisa wa kike kusifika, kupata umaarufu na kutamanika hadharani nchini Kenya. Kwa wengi huu ni utani tu. Haudhuru. Lakini je, kweli haudhuru? Bila shaka jibu la wafeministi kwa swali hili litakinzana na maoni na tabia za Wakenya wengi.