Urembo au Juhudi: Wanawake kwenye Idara ya Polisi, Kenya

Miaka michache iliyopita, afisa mmoja wa kike alipata umaarufu usiomidhilika. Umaarufu huu ulitokana, sio kutokana na kazi yake, bali ni kupitia urembo wa sura na umbile lake. Mwili wa afisa huyu ulijadiliwa, ukasifiwa, na kumezewa mate hadharani kwa siku kadhaa. Vile vile picha yake ilikatakatwa na kuhaririwa kwa jinsi tofauti ili kutosheleza matwaka ya wananchi haswa, nafikiri, wanaume. Ilishangaza sana kuona baadhi ya wanaume wakitamani hadharani kukamatwa na afisa huyo. Wengi walirai, “Tafathali nikamate!”